Mwa. 48:3-14 Swahili Union Version (SUV)

3. Yakobo akamwambia Yusufu, Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu, katika nchi ya Kanaani, akanibariki,

4. akaniambia, Mimi hapa, nitakuongezea uzao wako, na kukuzidisha, nami nitakufanya uwe kundi la mataifa; kisha nitawapa wazao wako nchi hii baada yako, iwe milki ya milele.

5. Basi sasa wanao wawili uliozaliwa katika nchi ya Misri kabla sijaja kwako Misri ni watoto wangu, yaani, Efraimu na Manase watakuwa wangu, kama Reubeni na Simeoni.

6. Na wazao wako utakaozaa baada ya hawa watakuwa wako; kwa jina la ndugu zao wataitwa katika urithi wao.

7. Na mimi nilipokuja kutoka Padan, Raheli akanifia katika nchi ya Kanaani, njiani, si mwendo mkubwa kabla ya kufika Efrathi. Nikamzika katika njia ya Efrathi, ndio Bethlehemu.

8. Israeli akawaona wana wa Yusufu, akasema, Ni nani hawa?

9. Yusufu akamwambia babaye, Hawa ni wanangu, Mungu alionipa hapa. Akasema, Tafadhali uwalete kwangu nami nitawabariki.

10. Na macho ya Israeli yalikuwa mazito kwa uzee, wala hakuweza kuona. Akawaleta kwake, naye akawabusu, na kuwakumbatia.

11. Israeli akamwambia Yusufu, Sikudhani ya kwamba nitakuona uso wako, na Mungu amenionyesha na uzao wako pia.

12. Yusufu akawatoa katika magoti yake, naye akainama kifudifudi

13. Yusufu akawaweka wote wawili, Efraimu katika mkono wake wa kuume, kuelekea mkono wa kushoto wa Israeli; na Manase katika mkono wake wa kushoto, kuelekea mkono wa kuume wa Israeli, akawasogeza karibu naye.

14. Israeli akanyosha mkono wake wa kuume akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, aliyekuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto akauweka juu ya kichwa cha Manase, huku akijua atiavyo mikono; maana Manase ndiye aliyezaliwa kwanza.

Mwa. 48