Mwa. 44:14-29 Swahili Union Version (SUV)

14. Akaja Yuda na ndugu zake nyumbani kwa Yusufu, naye mwenyewe alikuwamo, nao wakamwangukia kifudifudi.

15. Yusufu akawaambia, Ni tendo gani hili mlilolitenda? Hamkujua ya kwamba mtu kama mimi naweza kufanya uaguzi?

16. Yuda akasema, Tumwambie nini bwana wangu? Tusemeje! Tujivutieje haki? Mungu ameona uovu wa watumwa wako. Tazama, sisi ni watumwa wa bwana wangu, sisi na yeye ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake.

17. Akasema, Hasha! Nisifanye hivi; mtu ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake, ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Nanyi enendeni zenu kwa amani kwa baba yenu.

18. Ndipo Yuda akamkaribia, akasema, Tafadhali, bwana wangu, mtumwa wako na aseme neno moja masikioni mwa bwana wangu, wala hasira yako isimwakie mtumwa wako, maana wewe u kama Farao.

19. Wewe, bwana wangu, ulituuliza watumwa wako, ukisema, Je! Mnaye baba, au ndugu?

20. Tukakuambia wewe, bwana wangu, Tunaye baba, naye ni mzee, na mwana wa uzee wake ni mdogo, na nduguye amekufa; amebaki yeye peke yake wa katika tumbo la mamaye, na baba yake anampenda.

21. Ukatuambia watumwa wako, Mleteni kwangu, ili macho yangu yamwangalie.

22. Tukakuambia, bwana wangu, Kijana hawezi kumwacha babaye, maana akimwacha babaye, babaye atakufa.

23. Ukatuambia watumwa wako, Asiposhuka ndugu yenu mdogo pamoja nanyi, hamtaniona uso wangu tena

24. Ikawa tulipokwenda kwa mtumwa wako, baba yangu, tukamwarifu maneno yako, bwana wangu.

25. Kisha baba yetu akanena, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo.

26. Tukasema, Hatuwezi kwenda; ndugu yetu mdogo akiwapo pamoja nasi, tutashuka, maana hatutaweza kuuona uso wa mtu huyo, ndugu yetu mdogo asipokuwa pamoja nasi.

27. Mtumwa wako, baba yangu, akatuambia, Mnajua ya kuwa mke wangu alinizalia wana wawili;

28. mmoja alitoka kwangu, nikasema, Bila shaka ameraruliwa, wala sikumwona tangu hapo.

29. Na mkiniondolea huyu naye, na madhara yakimpata, mtashusha mvi zangu na msiba kaburini.

Mwa. 44