21. Wakaambiana, Kweli sisi tulimkosa ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi, wala hatukusikia kwa hiyo shida hii imetupata.
22. Reubeni akajibu, akawaambia, Sikuwaambia, nikisema, msimkose kijana? Wala hamkusikia; kwa hiyo damu yake inatakwa tena.
23. Wala hawakujua ya kwamba Yusufu anawasikia, kwa sababu alikuwapo mkalimani kati yao.
24. Akajitenga nao akalia. Kisha akawarudia, na kusema nao, akamtwaa Simeoni miongoni mwao, akamfunga mbele ya macho yao.
25. Yusufu akaamuru kuvijaza vyombo vyao nafaka, na kumrudishia kila mtu fedha yake katika gunia lake, na kuwapa chakula cha njiani.
26. Navyo ndivyo walivyofanyiwa. Wakaweka nafaka yao juu ya punda zao, wakatoka huko.
27. Mmoja wao alipofungua gunia lake ili ampe punda wake chakula katika nyumba ya wageni, aliiona fedha yake; kumbe! Iko kinywani mwa gunia lake.
28. Akawaambia nduguze, Fedha yangu imerudishwa, angalia, imo humo guniani mwangu. Mioyo yao ikazimia, wakageukiana wakitetemeka, wakasema, N’nini hii Mungu aliyotutendea?
29. Wakaja kwa Yakobo, baba yao, katika nchi ya Kanaani, wakampasha habari za yote yaliyowapata, wakisema,
30. Mtu yule aliye bwana wa nchi alisema nasi kwa maneno makali, akatufanya tu wapelelezi wa nchi.
31. Tukamwambia, Tu watu wa kweli sisi, wala si wapelelezi.
32. Sisi tu ndugu kumi na wawili, wana wa baba yetu. Mmoja hayuko, na mdogo wetu yuko pamoja na baba yetu leo katika nchi ya Kanaani.
33. Yule mtu, bwana wa nchi, akatuambia, Kwa njia hii nitawajua kama ninyi ni watu wa kweli; ndugu yenu mmoja mwacheni huku kwangu, kachukueni nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, mwende zenu.