Mwa. 41:4-20 Swahili Union Version (SUV)

4. Kisha hao ng’ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng’ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka.

5. Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema.

6. Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao.

7. Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu.

8. Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo.

9. Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema, Nayakumbuka makosa yangu leo.

10. Farao aliwakasirikia watumwa wake, akanitia nifungwe nyumbani mwa mkuu wa askari, mimi na mkuu wa waokaji.

11. Tukaota ndoto usiku mmoja, mimi na yeye; kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake tukaota.

12. Na huko pamoja nasi palikuwa na kijana; Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa askari, tukamhadithia, naye akatufasiria ndoto zetu; akamfasiria kila mtu kama ilivyokuwa ndoto yake.

13. Ikawa, kama vile alivyotufasiria ndivyo ilivyotokea; mimi nalirudishwa katika kazi yangu, na yeye alitundikwa.

14. Ndipo Farao akapeleka watu, akamwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao.

15. Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri.

16. Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani.

17. Farao akamwambia Yusufu, Katika ndoto yangu nalikuwa nikisimama ukingoni mwa mto;

18. na tazama, ng’ombe saba wanatoka mtoni, wanono, wazuri, wakajilisha manyasini.

19. Kisha, tazama, ng’ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu.

20. Na hao ng’ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng’ombe saba wa kwanza, wale wanono.

Mwa. 41