Mwa. 41:23-34 Swahili Union Version (SUV)

23. Na tazama, masuke saba membamba, dhaifu, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao.

24. Na hayo masuke dhaifu yakameza yale masuke saba mema. Nami nikawaambia hao waganga, wala hakuna aliyeweza kunionyesha maana yake.

25. Yusufu akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu.

26. Wale ng’ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja.

27. Na wale ng’ombe saba, dhaifu, wabaya, waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa.

28. Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu.

29. Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri.

30. Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi.

31. Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana.

32. Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi.

33. Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri.

34. Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba.

Mwa. 41