15. Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri.
16. Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani.
17. Farao akamwambia Yusufu, Katika ndoto yangu nalikuwa nikisimama ukingoni mwa mto;
18. na tazama, ng’ombe saba wanatoka mtoni, wanono, wazuri, wakajilisha manyasini.
19. Kisha, tazama, ng’ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu.
20. Na hao ng’ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng’ombe saba wa kwanza, wale wanono.
21. Na walipokwisha kuwala haikutambulikana ya kwamba wamewala, bali wakaonekana wabaya kama kwanza. Basi nikaamka.
22. Kisha nikaona katika ndoto yangu, na tazama, masuke saba yanatokeza katika bua moja, mema, yamejaa.
23. Na tazama, masuke saba membamba, dhaifu, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao.
24. Na hayo masuke dhaifu yakameza yale masuke saba mema. Nami nikawaambia hao waganga, wala hakuna aliyeweza kunionyesha maana yake.