Mwa. 4:11-22 Swahili Union Version (SUV)

11. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;

12. utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani.

13. Kaini akamwambia BWANA, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.

14. Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.

15. BWANA akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. BWANA akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga.

16. Kaini akatoka mbele za uso wa BWANA, akakaa katika nchi ya Nodi, mbele ya Edeni.

17. Kaini akamjua mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Henoko; akajenga mji akauita Henoko, kwa jina la mwanawe.

18. Henoko akamzaa Iradi, Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli; Methushaeli akamzaa Lameki.

19. Lameki akajitwalia wake wawili, jina la wa kwanza ni Ada, na jina la wa pili ni Sila.

20. Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama.

21. Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi.

22. Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake Tubal-kaini alikuwa Naama.

Mwa. 4