Mwa. 38:19-28 Swahili Union Version (SUV)

19. Akaondoka, akaenda zake, akavua utaji wake, na kuvaa mavazi ya ujane wake.

20. Yuda akapeleka yule mwana-mbuzi kwa mkono wa rafiki yake Mwadulami, ili aipate rehani mkononi mwa huyo mwanamke lakini hakumkuta.

21. Akauliza watu wa mahali pale, akisema, Yuko wapi yule kahaba aliyekuwapo Enaimu kando ya njia? Wakasema, Hakuwako hapa kahaba.

22. Akamrudia Yuda akasema, Sikumwona; hata na watu wa mahali hapo walisema, Hakuwako kahaba.

23. Yuda akasema, Na aichukue yeye, tusije tukatiwa aibu; tazama, nimempelekea mbuzi huyu, wala hukumkuta.

24. Ikawa baada ya miezi mitatu Yuda akapewa habari kwamba, Mkweo, Tamari, amefanya uzinifu, naye ana mimba ya haramu. Yuda akasema, Mtoeni ateketezwe.

25. Alipotolewa, alipeleka watu kwa mkwewe, akisema, Mimi nimepewa mimba na mtu mwenye vitu hivi. Akasema, Tambua basi, vitu hivi ni vya nani, pete hii, na kamba hii, na fimbo hii.

26. Yuda akavikiri, akasema, Yeye ni mwenye haki kuliko mimi, kwa kuwa sikumpa Shela, mwanangu. Wala hakumjua tena baada ya hayo.

27. Ikawa, wakati wake wa kuzaa walikuwapo mapacha tumboni mwake.

28. Ikawa alipokuwa akizaa, mtoto mmoja akatoa mkono, mzalisha akautwaa uzi mwekundu akaufunga mkononi mwake, huku akisema, Huyu ametoka kwanza.

Mwa. 38