Mwa. 37:17-27 Swahili Union Version (SUV)

17. Yule mtu akasema, Wametoka hapa, maana niliwasikia wakisema, Twendeni Dothani. Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani.

18. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue.

19. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja.

20. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.

21. Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue.

22. Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika birika hii iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake.

23. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa,

24. wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji.

25. Nao wakakaa kitako kula chakula; wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri.

26. Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake?

27. Haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yetu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali.

Mwa. 37