1. Yakobo akainua macho yake, akaona, na tazama, Esau anakuja na watu mia nne pamoja naye. Akawagawanyia Lea, na Raheli, na wale vijakazi wawili, wana wao.
2. Akawaweka hao vijakazi na wana wao mbele, na Lea na wanawe nyuma yao, na Raheli na Yusufu mwisho.
3. Akapita mwenyewe mbele yao, akainama mpaka nchi mara saba, hata alipomkaribia ndugu yake.
4. Esau akaja mbio kumlaki, akamkumbatia, na kumwangukia shingoni, akambusu; nao wakalia.
5. Akainua macho yake, akawaona wale wanawake na watoto, akauliza, Ni nani hawa walio pamoja nawe? Akasema, Ni watoto Mungu aliompa mtumwa wako kwa neema yake.
6. Ndipo wale vijakazi, na wana wao, wakakaribia wakainama.
7. Lea naye, na wanawe, wakakaribia wakainama. Baadaye Yusufu na Raheli wakakaribia, wakainama.