Mwa. 30:32-43 Swahili Union Version (SUV)

32. Nitapita katika wanyama wako wote leo, na kutoa huko kila mnyama aliye na madoadoa na marakaraka, na kila mnyama mweusi katika hao kondoo, na aliye na marakaraka na madoadoa katika mbuzi; nao watakuwa mshahara wangu.

33. Na haki yangu itanishuhudia katika siku zijazo, utakapokuja kwa habari ya mshahara wangu ulioko kwako. Kila asiye madoadoa au marakaraka katika mbuzi, au asiye mweusi katika kondoo, akionekana kwangu, itahesabiwa kuwa ameibiwa.

34. Labani akasema, Tazama, na iwe hivi kama usemavyo.

35. Basi akatoa siku ile mbuzi waume walio na milia na madoadoa, na mbuzi wake walio na madoadoa na marakaraka, kila aliye na doa jeupe, na kondoo wote waliokuwa weusi, akawatia mikononi mwa wanawe.

36. Akajitenga na Yakobo mwendo wa siku tatu; naye Yakobo akachunga wanyama wa Labani waliosalia.

37. Yakobo akatwaa fito za mlubna mbichi, na mlozi, na mwaramoni, akazibambua maganda, mistari myeupe ionekane ndani ya hizo fito.

38. Akazisimamisha fito hizo alizozibambua katika mabirika ya kunyweshea maji, pale walipokuja wanyama wanywe; wakachukua mimba walipokuja kunywa.

39. Wanyama wakapata mimba mbele ya hizo fito, wakazaa wanyama walio na milia, na madoadoa, na marakaraka.

40. Na Yakobo akawatenga wana-kondoo, akazielekeza nyuso za makundi zielekee wale waliokuwa na milia, na kila aliyekuwa mweusi katika wanyama wa Labani. Akaweka kando wanyama wake mwenyewe, wala hakuwachanganya pamoja na wanyama wa Labani.

41. Ikawa kila walipopata mimba wanyama wenye nguvu, Yakobo akaziweka zile fito mbele ya macho ya hao wanyama katika mabirika ili kwamba wachukue mimba kati ya zile fito,

42. lakini wanyama walipodhoofika hakuziweka zile fito. Basi wale dhaifu walikuwa wa Labani, na wenye nguvu walikuwa wa Yakobo.

43. Kwa hiyo mtu huyo akazidi mno, akawa na wanyama wengi, na vijakazi, na watumwa, na ngamia, na punda.

Mwa. 30