Mwa. 30:20-37 Swahili Union Version (SUV)

20. Lea akasema, Mungu amenipa mahari njema, sasa mume wangu atakaa nami, kwa kuwa nimemzalia wana sita. Akamwita jina lake Zabuloni.

21. Baadaye akazaa binti, akamwita jina lake Dina.

22. Mungu akamkumbuka Raheli; Mungu akamsikia, akamfungua tumbo.

23. Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, Mungu ameondoa aibu yangu.

24. Akamwita jina lake Yusufu, akisema, Bwana aniongeze mwana mwingine.

25. Ikawa Raheli alipomzaa Yusufu, Yakobo akamwambia Labani, Nipe ruhusa niende kwetu, na kwenye nchi yangu.

26. Nipe wake zangu na watoto wangu, niliokutumikia, niende zangu, maana umejua utumishi wangu niliokutumikia.

27. Labani akamwambia, Iwapo nimeona fadhili machoni pako, kaa, maana nimetambua ya kwamba BWANA amenibariki kwa ajili yako.

28. Akasema, Sema mshahara wako utakao, nami nitatoa.

29. Akamwambia, Umejua jinsi nilivyokutumikia, na jinsi wanyama wako walivyokuwa kwangu.

30. Maana mali yako ilikuwa haba kabla sijaja, nayo imezidi kuwa nyingi, BWANA akakubariki kila nilikokwenda. Basi sasa, nitaangalia lini mambo ya nyumba yangu mwenyewe?

31. Akamwuliza, Nikupe nini? Yakobo akasema, Usinipe kitu; ukinifanyia neno hili, nitalisha wanyama wako tena na kuwalinda.

32. Nitapita katika wanyama wako wote leo, na kutoa huko kila mnyama aliye na madoadoa na marakaraka, na kila mnyama mweusi katika hao kondoo, na aliye na marakaraka na madoadoa katika mbuzi; nao watakuwa mshahara wangu.

33. Na haki yangu itanishuhudia katika siku zijazo, utakapokuja kwa habari ya mshahara wangu ulioko kwako. Kila asiye madoadoa au marakaraka katika mbuzi, au asiye mweusi katika kondoo, akionekana kwangu, itahesabiwa kuwa ameibiwa.

34. Labani akasema, Tazama, na iwe hivi kama usemavyo.

35. Basi akatoa siku ile mbuzi waume walio na milia na madoadoa, na mbuzi wake walio na madoadoa na marakaraka, kila aliye na doa jeupe, na kondoo wote waliokuwa weusi, akawatia mikononi mwa wanawe.

36. Akajitenga na Yakobo mwendo wa siku tatu; naye Yakobo akachunga wanyama wa Labani waliosalia.

37. Yakobo akatwaa fito za mlubna mbichi, na mlozi, na mwaramoni, akazibambua maganda, mistari myeupe ionekane ndani ya hizo fito.

Mwa. 30