15. Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Ibrahimu, naye ana mtungi begani pake.
16. Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda.
17. Ndipo yule mtumishi akapiga mbio kwenda kumlaki, akasema, Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe.
18. Naye akasema, Unywe, bwana wangu, akafanya haraka, akatua mtungi wake mkononi mwake, akamnywesha.
19. Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa.
20. Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote.
21. Basi yule mtu akamkazia macho, akanyamaza, ili ajue kwamba BWANA ameifanikisha safari yake ama sivyo.
22. Ikawa, ngamia walipokwisha kunywa, yule mtu akatwaa pete ya dhahabu, uzani wake ulikuwa nusu shekeli, na vikuku viwili kwa mikono yake, uzani wake ulikuwa shekeli kumi za dhahabu,
23. akasema, U binti wa nani wewe? Tafadhali uniambie. Je! Iko nafasi katika nyumba ya baba yako tupate mahali pa kukaa kwa muda?
24. Akasema, Mimi ni binti wa Bethueli mwana wa Milka, aliyemzalia Nahori.
25. Tena akamwambia, Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha, na mahali pa kukaa wageni.
26. Yule mtu akainama akamsujudu BWANA.
27. Akasema, Na atukuzwe BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ambaye hakuacha rehema zake na kweli yake kwa bwana wangu. BWANA akaniongoza mimi nami njiani hata nyumba ya nduguze bwana wangu.
28. Basi yule msichana akapiga mbio, akawaambia watu wa nyumba ya mama yake mambo hayo.
29. Na Rebeka alikuwa na kaka, jina lake Labani. Labani akatoka mbio kumwendea yule mtu kisimani.
30. Ikawa, alipoiona ile pete, na vikuku mikononi mwa nduguye, akasikia maneno ya Rebeka nduguye, akisema, Hivyo ndivyo alivyoniambia mtu huyo, basi akamjia mtu yule, na tazama, amesimama karibu na ngamia kisimani.
31. Akasema, Karibu, wewe uliyebarikiwa na BWANA, mbona unasimama nje? Kwa maana nimeiweka nyumba tayari, na nafasi kwa ngamia.