Mwa. 23:4-11 Swahili Union Version (SUV)

4. Mimi ni mgeni, ninatembea kwenu; nipeni mahali pa kuzikia kwenu, pawe pangu, nimzike maiti wangu atoke mbele yangu.

5. Wazawa wa Hethi wakamjibu Ibrahimu, wakamwambia,

6. Utusikie, Ee bwana, ndiwe mtu mkuu sana kwetu, uzike maiti wako katika kaburi lile utakalochagua katika makaburi yetu. Hapana mtu kwetu atakayekuzuilia kaburi lake, usizike maiti wako.

7. Ibrahimu akaondoka, akainama mbele ya watu wa nchi, mbele ya hao wazawa wa Hethi.

8. Naye akazungumza nao, akisema, Ikiwa nia yenu nimzike maiti wangu atoke mbele yangu, mnisikie, mkaniombee kwa Efroni bin Sohari,

9. ili kwamba anipe pango ya Makpela, iliyo katika mpaka wa shamba lake, na anipe kwa kima kilicho kamili, katikati yenu, iwe milki yangu ya kuzikia.

10. Basi Efroni alikuwa akiketi kati ya wazawa wa Hethi. Efroni Mhiti akamjibu Ibrahimu, na wazawa wa Hethi wanasikiliza, hata watu wote waingiao mlango wa mji wake, akisema,

11. Sivyo, bwana wangu, unisikilize. Lile shamba nakupa, na pango iliyomo nakupa; mbele ya wana wa watu wangu nakupa, uzike maiti wako.

Mwa. 23