Mwa. 21:18-27 Swahili Union Version (SUV)

18. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa.

19. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana.

20. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde.

21. Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri.

22. Ikawa wakati ule Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakamwambia Ibrahimu, wakinena, Mungu yu pamoja nawe katika yote unayotenda.

23. Basi sasa uniapie kwa Mungu, ya kuwa hutanitenda hila, wala mwanangu, wala mjukuu wangu, lakini kwa kadiri ya fadhili niliyokutendea utanitendea mimi, na nchi hii ambayo umetembea ndani yake.

24. Ibrahimu akasema, Nitaapa.

25. Kisha Ibrahimu akamlaumu Abimeleki kwa sababu ya kisima cha maji ambacho watumwa wa Abimeleki wamekinyang’anya.

26. Abimeleki akasema, Mimi sijui ni nani aliyetenda neno hili, wala hukuniambia, wala sikusikia habari hii ila leo tu.

27. Ibrahimu akatwaa kondoo na ng’ombe akampa Abimeleki, na hao wawili wakafanya mapatano.

Mwa. 21