Mwa. 20:1-11 Swahili Union Version (SUV)

1. Ibrahimu akaondoka huko kwenda nchi ya kusini, akakaa kati ya Kadeshi na Shuri, naye akatembea katika Gerari.

2. Ibrahimu akamnena Sara mkewe, Huyu ni ndugu yangu. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akapeleka watu akamtwaa Sara.

3. Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu.

4. Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee Bwana, Je! Utaua hata taifa lenye haki?

5. Je! Hakuniambia mwenyewe, Huyu ni ndugu yangu? Na mwanamke mwenyewe naye alisema, Huyu ni ndugu yangu. Kwa ukamilifu wa moyo wangu, na kwa kuwa safi mikono yangu, nimefanya hivi.

6. Mungu akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse.

7. Basi sasa umrudishe mwanamke kwa mtu huyo, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate kuishi. Bali usipomrudisha, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu wote ulio nao.

8. Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumwa wake wote, akawaambia maneno hayo yote masikioni mwao, nao watu hao wakaogopa sana.

9. Kisha Abimeleki akamwita Ibrahimu, akamwambia, Umetutenda nini? Nimekukosa nini, hata ukaleta juu yangu na juu ya ufalme wangu dhambi kuu? Umenitenda matendo yasiyotendeka.

10. Abimeleki akamwambia Ibrahimu, Umeona nini hata ukatenda jambo hili?

11. Ibrahimu akasema, Kwa sababu naliona, Yakini hapana hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa ajili ya mke wangu.

Mwa. 20