Mwa. 17:11-27 Swahili Union Version (SUV)

11. Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi.

12. Mtoto wa siku nane atatahiriwa kwenu, kila mwanamume katika vizazi vyenu, mzaliwa nyumbani, na mnunuliwa kwa fedha, kila mgeni asiyekuwa wa uzao wako.

13. Mzaliwa nyumbani mwako, na mnunuliwa kwa fedha yako, lazima atahiriwe; na agano langu litakuwa katika mwili wenu, kuwa agano la milele.

14. Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu yule atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu.

15. Mungu akamwambia Ibrahimu, Sarai mkeo, hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa jina lake litakuwa Sara.

16. Nami nitambariki, na tena nitakupa mwana kwake, naam, nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa, na wafalme wa kabila za watu watatoka kwake.

17. Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema moyoni, Je! Mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa miaka tisini atazaa?

18. Ibrahimu akamwambia Mungu, Lau kwamba Ishmaeli angeishi mbele yako.

19. Mungu akasema, Sivyo, lakini Sara mkeo atakuzalia mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Isaka. Nami nitafanya agano langu imara kwake kuwa agano la milele kwa ajili ya uzao wake baada yake.

20. Na kwa habari za Ishmaeli nimekusikia, nimembariki, nitamzidisha, nami nitamwongeza sana sana. Atazaa maseyidi kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kuu.

21. Bali agano langu nitalifanya imara kwa Isaka, ambaye Sara atakuzalia majira kama haya mwaka ujao.

22. Mungu akaacha kusema naye, akapanda kutoka kwa Ibrahimu.

23. Ibrahimu akamtwaa Ishmaeli mwanawe, na wote waliozaliwa nyumbani mwake, na wote walionunuliwa kwa fedha yake, wanaume wote wa watu wa nyumba ya Ibrahimu, akawatahiri nyama ya magovi yao siku ile ile, kama Mungu alivyomwambia.

24. Naye Ibrahimu alikuwa mwenye umri wa miaka tisini na kenda alipotahiriwa nyama ya govi lake.

25. Na Ishmaeli mwanawe alikuwa mtu wa miaka kumi na mitatu, alipotahiriwa nyama ya govi lake.

26. Siku ile ile akatahiriwa Ibrahimu na Ishmaeli mwanawe.

27. Na watu wote wa nyumba yake, wazaliwa nyumbani, na wanunuliwa kwa fedha katika mkono wa mgeni, wakatahiriwa pamoja naye.

Mwa. 17