Mwa. 13:8-18 Swahili Union Version (SUV)

8. Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu ndugu.

9. Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi ujitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kuume; ukienda upande wa kuume, nitakwenda upande wa kushoto.

10. Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari.

11. Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao.

12. Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma.

13. Lakini watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya BWANA.

14. BWANA akamwambia Abramu, alipokwisha kutengana na Lutu, Inua sasa macho yako, ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini, na wa kusini na wa mashariki na wa magharibi;

15. maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele.

16. Na uzao wako nitaufanya uwe kama mavumbi ya nchi; hata mtu akiweza kuyahesabu mavumbi ya nchi, uzao wako nao utahesabika.

17. Ondoka, ukatembee katika nchi hii katika mapana yake, na marefu yake, maana nitakupa wewe nchi hiyo.

18. Basi Abramu akajongeza hema yake, akaja akakaa kwenye mialoni ya Mamre, nayo ni miti iliyoko Hebroni, akamjengea BWANA madhabahu huko.

Mwa. 13