5. Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaani.
6. Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali patakatifu pa Shekemu; mpaka mwaloni wa More. Na Wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo.
7. BWANA akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu BWANA aliyemtokea.
8. Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea BWANA madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA.
9. Naye Abramu akasafiri, akazidi kwenda pande za kusini.
10. Basi kulikuwa njaa katika nchi ile; Abramu akashuka Misri, akae huko kwa muda maana njaa ilikuwa nzito katika nchi.
11. Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso;
12. basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai.
13. Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako.