7. Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake.
8. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii.
9. Naye Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata.
10. Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake.
11. Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?
12. Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi.
13. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.
14. Wakati ule wanafunzi wake Yohana wakamwendea, wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi?
15. Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga.
16. Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi.
17. Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote.
18. Alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi.
19. Akaondoka Yesu, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake.
20. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake.
21. Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona.
22. Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile.