16. Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi.
17. Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote.
18. Alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi.
19. Akaondoka Yesu, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake.
20. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake.
21. Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona.
22. Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile.
23. Yesu alipofika nyumbani kwa yule jumbe, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo,
24. akawaambia, Ondokeni; kwa maana kijana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana.
25. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule kijana akasimama.
26. Zikaenea habari hizi katika nchi ile yote.
27. Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi.
28. Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana.
29. Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu mpate.
30. Macho yao yakafumbuka. Naye Yesu akawaagiza kwa nguvu, akisema, Angalieni hata mtu mmoja asijue.
31. Lakini wakatoka, wakaeneza habari zake katika nchi ile yote.
32. Hata hao walipokuwa wakitoka, tazama, walimletea mtu bubu mwenye pepo.
33. Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wakastajabu, wakasema, Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wo wote.
34. Lakini Mafarisayo wakasema, Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo.