1. Naye alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia;
2. akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema,
3. Heri walio maskini wa roho;Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
4. Heri wenye huzuni;Maana hao watafarijika.
5. Heri wenye upole;Maana hao watairithi nchi.
6. Heri wenye njaa na kiu ya haki;Maana hao watashibishwa.
7. Heri wenye rehema;Maana hao watapata rehema.
8. Heri wenye moyo safi;Maana hao watamwona Mungu.
9. Heri wapatanishi;Maana hao wataitwa wana wa Mungu.
10. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki;Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
11. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu.
12. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.