Mt. 27:51-65 Swahili Union Version (SUV)

51. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;

52. makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;

53. nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi.

54. Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.

55. Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, hao ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia.

56. Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.

57. Hata ilipokuwa jioni akafika mtu tajiri wa Arimathaya, jina lake Yusufu, naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu;

58. mtu huyu alimwendea Pilato akauomba mwili wa Yesu. Ndipo Pilato akaamuru apewe.

59. Yusufu akautwaa mwili, akauzonga-zonga katika sanda ya kitani safi,

60. akauweka katika kaburi lake jipya, alilokuwa amelichonga mwambani; akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake.

61. Na pale walikuwapo Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, wameketi kulielekea kaburi.

62. Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato,

63. wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka.

64. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza.

65. Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo.

Mt. 27