46. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?
47. Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya.
48. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha.
49. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa.
50. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.
51. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;
52. makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;
53. nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi.
54. Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.
55. Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, hao ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia.
56. Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.
57. Hata ilipokuwa jioni akafika mtu tajiri wa Arimathaya, jina lake Yusufu, naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu;
58. mtu huyu alimwendea Pilato akauomba mwili wa Yesu. Ndipo Pilato akaamuru apewe.
59. Yusufu akautwaa mwili, akauzonga-zonga katika sanda ya kitani safi,
60. akauweka katika kaburi lake jipya, alilokuwa amelichonga mwambani; akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake.
61. Na pale walikuwapo Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, wameketi kulielekea kaburi.