40. Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani.
41. Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe.
42. Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini.
43. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu.
44. Pia wale wanyang’anyi waliosulibiwa pamoja naye walimshutumu vile vile.
45. Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa.
46. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?
47. Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya.
48. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha.
49. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa.
50. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.
51. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;
52. makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;