24. Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lo lote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe.
25. Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.
26. Ndipo akawafungulia Baraba; na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa ili asulibiwe.
27. Ndipo askari wa liwali wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima.
28. Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu.
29. Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi!
30. Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampiga-piga kichwani.
31. Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulibisha.
32. Hata walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha auchukue msalaba wake.
33. Na walipofika mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa,
34. wakampa kunywa divai iliyochanganyika na nyongo; lakini yeye alipoionja hakutaka kunywa.
35. Walipokwisha kumsulibisha, waligawa mavazi yake, wakipiga kura; [ili litimie neno lililonenwa na nabii, Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi langu walipiga kura.]
36. Wakaketi, wakamlinda huko.