Mt. 27:2-16 Swahili Union Version (SUV)

2. wakamfunga, wakamchukua, wakampeleka kwa Pilato aliyekuwa liwali.

3. Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia.

4. Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe.

5. Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga.

6. Wakuu wa makuhani wakavitwaa vile vipande vya fedha, wakasema, Si halali kuviweka katika sanduku ya sadaka, kwa kuwa ni kima cha damu.

7. Wakafanya shauri, wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni.

8. Kwa hiyo konde lile huitwa konde la damu hata leo.

9. Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Wakavitwaa vipande thelathini vya fedha, kima chake aliyetiwa kima, ambaye baadhi ya Waisraeli walimtia kima;

10. wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza.

11. Naye Yesu akasimama mbele ya liwali; liwali akamwuliza, akasema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Yesu akamwambia, Wewe wasema.

12. Lakini aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu hata neno.

13. Ndipo Pilato akamwambia, Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia?

14. Asimjibu hata neno moja, hata liwali akastaajabu sana.

15. Basi wakati wa siku kuu, liwali desturi yake huwafungulia mkutano mfungwa mmoja waliyemtaka.

16. Basi palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba.

Mt. 27