Mt. 26:8-20 Swahili Union Version (SUV)

8. Wanafunzi wake walipoona, wakachukiwa, wakasema, Ni wa nini upotevu huu?

9. Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa fedha nyingi wakapewa maskini.

10. Yesu akatambua akawaambia, Mbona mnamtaabisha mwanamke? Maana ni kazi njema aliyonitendea mimi.

11. Kwa maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi; lakini mimi hamnami siku zote.

12. Maana kwa kunimwagia mwili wangu marhamu hiyo, ametenda hivyo ili kuniweka tayari kwa maziko yangu.

13. Amin, nawaambieni, Kila patakapohubiriwa Injili hii katika ulimwengu wote, tendo hilo alilolitenda huyu litatajwa pia kwa kumbukumbu lake.

14. Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani,

15. akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha.

16. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti.

17. Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka?

18. Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu.

19. Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka.

20. Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara.

Mt. 26