Mt. 26:21-40 Swahili Union Version (SUV)

21. Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti.

22. Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana?

23. Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti.

24. Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa.

25. Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.

26. Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu

27. Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki;

28. kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.

29. Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.

30. Nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni.

31. Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika.

32. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.

33. Petro akajibu, akamwambia, Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe.

34. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, usiku huu kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu.

35. Petro akamwambia, Ijaponipasa kufa nawe, sitakukana kamwe. Na wanafunzi wote wakasema vivyo hivyo.

36. Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe.

37. Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka.

38. Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.

39. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.

40. Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?

Mt. 26