10. Yesu akatambua akawaambia, Mbona mnamtaabisha mwanamke? Maana ni kazi njema aliyonitendea mimi.
11. Kwa maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi; lakini mimi hamnami siku zote.
12. Maana kwa kunimwagia mwili wangu marhamu hiyo, ametenda hivyo ili kuniweka tayari kwa maziko yangu.
13. Amin, nawaambieni, Kila patakapohubiriwa Injili hii katika ulimwengu wote, tendo hilo alilolitenda huyu litatajwa pia kwa kumbukumbu lake.
14. Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani,
15. akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha.
16. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti.
17. Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka?
18. Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu.
19. Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka.
20. Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara.
21. Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti.
22. Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana?
23. Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti.
24. Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa.
25. Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.
26. Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu
27. Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki;