7. Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao.
8. Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.
9. Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.
10. Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa.
11. Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.
12. Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.
13. Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.
14. Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake.
15. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.
16. Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano.
17. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida.
18. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake.
19. Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao.
20. Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida.
21. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.
22. Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida.