9. Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu.
10. Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana.
11. Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi.
12. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa.
13. Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.
14. Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.
15. Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu),
16. ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani;
17. naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake;
18. wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake.
19. Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo!
20. Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.
21. Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe.
22. Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo.