Mt. 24:20-34 Swahili Union Version (SUV)

20. Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.

21. Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe.

22. Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo.

23. Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki.

24. Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.

25. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele.

26. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki.

27. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.

28. Kwa kuwa po pote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.

29. Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika;

30. ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.

31. Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu.

32. Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu;

33. nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni.

34. Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia.

Mt. 24