5. Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao;
6. hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi,
7. na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi.
8. Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu.
9. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni.
10. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo.
11. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu.
12. Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.
13. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie.
14. [Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnakula nyumba za wajane, na kwa unafiki mnasali sala ndefu; kwa hiyo mtapata hukumu iliyo kubwa zaidi.]
15. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanum mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe.
16. Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga.
17. Wapumbavu ninyi na vipofu; maana ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au lile hekalu liitakasalo dhahabu?