15. Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno.
16. Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu.
17. Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo?
18. Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki?
19. Nionyesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari.
20. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii?
21. Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu.
22. Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao.
23. Siku ile Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza,
24. wakisema, Mwalimu, Musa alisema, Mtu akifa, akiwa hana watoto, ndugu yake na amwoe yule mkewe, ili ampatie nduguye mzao.
25. Basi, kwetu kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akaoa, akafariki, na kwa kuwa hana mzao, akamwachia nduguye mke wake.