10. Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni.
11. Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi.
12. Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa.
13. Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
14. Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.
15. Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno.
16. Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu.
17. Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo?
18. Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki?
19. Nionyesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari.
20. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii?
21. Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu.
22. Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao.