1. Yesu akajibu, akawaambia tena kwa mithali, akisema,
2. Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi.
3. Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja.
4. Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng’ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini.
5. Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake;
6. nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua.
7. Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao.
8. Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili.
9. Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini.