5. Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile vile.
6. Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?
7. Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu.
8. Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza.
9. Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila mtu dinari.
10. Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari.
11. Basi wakiisha kuipokea, wakamnung’unikia mwenye nyumba,
12. wakisema, Hao wa mwisho wametenda kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana kutwa.
13. Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari?
14. Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.