3. Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi;
4. na hao nao akawaambia, Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda.
5. Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile vile.
6. Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?
7. Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu.
8. Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza.
9. Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila mtu dinari.
10. Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari.
11. Basi wakiisha kuipokea, wakamnung’unikia mwenye nyumba,
12. wakisema, Hao wa mwisho wametenda kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana kutwa.
13. Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari?
14. Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.
15. Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema?
16. Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.
17. Hata Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia,
18. Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi; nao watamhukumu afe;
19. kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeledi, na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka.
20. Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno.
21. Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako.
22. Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza.