Mt. 2:16-22 Swahili Union Version (SUV)

16. Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi.

17. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema,

18. Sauti ilisikiwa Rama,Kilio, na maombolezo mengi,Raheli akiwalilia watoto wake,Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako.

19. Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri,

20. akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto.

21. Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli.

22. Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya,

Mt. 2