Mt. 17:5-18 Swahili Union Version (SUV)

5. Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.

6. Na wale wanafunzi waliposikia, walianguka kifulifuli, wakaogopa sana.

7. Yesu akaja, akawagusa, akasema, Inukeni, wala msiogope.

8. Wakainua macho yao, wasione mtu ila Yesu peke yake.

9. Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu ye yote habari ya maono hayo, hata Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu.

10. Wanafunzi wake wakamwuliza, wakisema, Basi kwa nini waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza?

11. Naye akajibu, akawaambia, Kweli Eliya yuaja kwanza, naye atatengeneza yote,

12. ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha kuja, wasimtambue, lakini wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu naye yuaenda kuteswa kwao.

13. Ndipo wale wanafunzi walipofahamu ya kuwa amesema nao habari za Yohana Mbatizaji.

14. Nao walipoufikia mkutano, mtu mmoja akamjia, akampigia magoti, akisema,

15. Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini.

16. Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya.

17. Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu.

18. Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile.

Mt. 17