Mt. 16:5-22 Swahili Union Version (SUV)

5. Nao wanafunzi wakaenda hata ng’ambo, wakasahau kuchukua mikate.

6. Yesu akawaambia, Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.

7. Wakabishana wao kwa wao, wakisema, Ni kwa sababu hatukuchukua mikate.

8. Naye Yesu akafahamu, akawaambia, Mbona mnabishana ninyi kwa ninyi, enyi wa imani chache, kwa sababu hamna mikate?

9. Hamjafahamu bado, wala hamkumbuki ile mikate mitano kwa wale elfu tano, na vikapu vingapi mlivyoviokota?

10. Wala ile mikate saba kwa watu elfu nne, na makanda mangapi mliyoyaokota?

11. Imekuwaje hamkufahamu ya kuwa si kwa sababu ya mkate naliwaambia? Ila jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.

12. Ndipo walipofahamu ya kuwa hakuwaambia kujilinda na chachu ya mkate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.

13. Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?

14. Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.

15. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?

16. Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.

17. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.

18. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.

19. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.

20. Ndipo alipowakataza sana wanafunzi wake wasimwambie mtu ye yote ya kwamba yeye ndiye Kristo.

21. Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka.

22. Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.

Mt. 16