Mt. 16:1-8 Swahili Union Version (SUV)

1. Wakamjia Mafarisayo na Masadukayo, wakamjaribu, wakamwomba awaonyeshe ishara itokayo mbinguni.

2. Akajibu, akawaambia, [Kukiwa jioni, mwasema, Kutakuwa na kianga; kwa maana mbingu ni nyekundu.

3. Na asubuhi, mwasema, Leo kutakuwa na dhoruba; kwa maana mbingu ni nyekundu, tena kumetanda. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa mbingu; lakini, je! Ishara za zamani hizi hamwezi kuzitambua?]

4. Kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya Yona. Akawaacha, akaenda zake.

5. Nao wanafunzi wakaenda hata ng’ambo, wakasahau kuchukua mikate.

6. Yesu akawaambia, Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.

7. Wakabishana wao kwa wao, wakisema, Ni kwa sababu hatukuchukua mikate.

8. Naye Yesu akafahamu, akawaambia, Mbona mnabishana ninyi kwa ninyi, enyi wa imani chache, kwa sababu hamna mikate?

Mt. 16