20. hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula kabla hajanawa mikono hakumtii mtu unajisi.
21. Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni.
22. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.
23. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.
24. Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.
25. Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie.
26. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.
27. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.
28. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.
29. Yesu akaondoka huko, akafika kando ya bahari ya Galilaya; akapanda mlimani, akaketi huko.
30. Wakamwendea makutano mengi wakimletea viwete, vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; akawaponya;
31. hata ule mkutano wakastaajabu, walipowaona mabubu wanasema, vilema wanakuwa wazima, viwete wanakwenda, na vipofu wanaona; wakamtukuza Mungu wa Israeli.
32. Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema, Nawahurumia mkutano, kwa kuwa yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena kuwaaga wakifunga sipendi, wasije wakazimia njiani.
33. Wanafunzi wake wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii?
34. Yesu akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, na visamaki vichache.