1. Wakati ule mfalme Herode alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake,
2. Huyo ndiye Yohana Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake.
3. Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye.
4. Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye.
5. Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohana kuwa nabii.
6. Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode.
7. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote atakaloliomba.
8. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji.
9. Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe;
10. akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani.
11. Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana; akakichukua kwa mamaye.
12. Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari.
13. Naye Yesu aliposikia; hayo, aliondoka huko katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao.