30. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.
31. Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake;
32. nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake.
33. Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia.
34. Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno;
35. ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema,Nitafumbua kinywa changu kwa mifano,Nitayatamka yaliyositirika tangu awali.
36. Kisha Yesu akawaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni.
37. Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu;
38. lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu;
39. yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika.