25. Ndipo akaweka tena mikono yake juu ya macho yake, naye akatazama sana; akawa mzima, akaona vyote waziwazi.
26. Akampeleka nyumbani kwake, akisema, Hata kijijini usiingie.
27. Akatoka Yesu na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria-Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, Watu huninena mimi kuwa ni nani?
28. Wakamjibu, Yohana Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii.
29. Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo.
30. Akawaonya wasimwambie mtu habari zake.
31. Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka.
32. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua, akaanza kumkemea.
33. Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.
34. Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.