20. Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi.
21. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati,
22. wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu.
23. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.
24. Akaondoka huko, akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba, akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika.
25. Ila mara mwanamke, ambaye binti yake yuna pepo mchafu, alisikia habari zake, akaja akamwangukia miguuni pake.
26. Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika binti yake.
27. Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa.
28. Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto.
29. Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, enenda zako, pepo amemtoka binti yako.