Mk. 7:10-19 Swahili Union Version (SUV)

10. Maana Musa alisema, Waheshimu baba yako na mama yako, na, Amtukanaye babaye au mamaye kufa na afe.

11. Bali ninyi husema, Mtu akimwambia babaye au mamaye, Ni Korbani, yaani, wakfu, kitu changu cho chote kikupasacho kufaidiwa nacho, huwa basi;

12. wala hammruhusu baada ya hayo kumtendea neno babaye au mamaye;

13. huku mkilitangua neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo mengi yaliyo sawasawa na hayo.

14. Akawaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu.

15. Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu. [

16. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.]

17. Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano.

18. Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi;

19. kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote.

Mk. 7