1. Kisha Mafarisayo, na baadhi ya waandishi waliotoka Yerusalemu, wakakusanyika mbele yake,
2. wakaona wengine katika wanafunzi wake wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa.
3. Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao;
4. tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea kuyashika, kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba.
5. Basi wale Mafarisayo na waandishi wakamwuliza, Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi?